Mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari Gerezani, Shakil Sures amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya kujeruhiwa kwa risasi na polisi kwenye mazingira ya kutatanisha. Tukio hilo lililotokea Jumatatu eneo la Fire, Upanga licha ya watu kusikia milio ya risasi, kushuhudia polisi wakipita na kumuona kijana huyo akiwa tayari kajeruhiwa, lakini hakuna mwenye maelezo sahihi kuhusu nini kilitokea hadi askari hao wakachukua hatua hiyo. Baadhi ya waliokuwapo eneo la tukio siku hiyo walidai kuwaona askari waliokuwa eneo hilo wakirusha risasi, bila kujua walikuwa wakipambana na nani. Mmoja wa mashuhuda, Athumani Simba alidai walidhani ni majibizano ya risasi kati ya askari na majambazi, baada ya kuona gari la polisi likipita eneo hilo. “Niliwaona askari wawili wakielekea eneo la Fire huku wakipiga risasi, ghafla nilimuona mwanafunzi akilia huku akiwa ameshika mguu wake akiomba msaada,” alisema Simba. Ofisa U...