Skip to main content

TAFSIRI NA UKALIMANI

 

1.Dhana ya Tafsiri.

Tafsiri imefasiliwa kuwa, ni Kutoa mawazo kutoka katika lugha moja kwenda lugha nyingine bila ya kubadilisha maana. [TUKI 2002: 271]

Mwansoko na wenzake (2006), wanafasili tafsiri kuwa ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine.

Catford [1965:20] anasema tafsiri ni, “Kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja {lugha chanzi} na kuweka badala yake mawazo yanayolingana katika lugha nyingine {lugha lengwa}.

AS-Safi akimnukuu Dubois (1974), anaeleza kuwa tafsiri ni uelezaji katika lugha nyingine au lugha lengwa wa kile kilichoelezwa katika lugha nyingine (lugha chanzi) ikihifadhi maana na mtindo wa matini chanzi.

            Maana zote hizo tulizoziangalia, utaona kuwa, kuna mambo matatu muhimu yanayojitokeza, mambo hayo ni:

(i) Mawazo yanayotakiwa kutafsiriwa sharti yawe katika maandishi.

(ii) Mawazo au ujumbe kati ya lugha chanzi na lugha lengwa sharti yalingane.

(iii) Tafsiri inaweza kuwa kutoa maana ya maneno au mawazo.

Kutokana na fasili hizo tunaweza kusema kuwa tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo, ujumbe, au taarifa iliyopo katika maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa bila kupoteza maana ya msingi na mtindo uliotumika katika matini chanzi.

   Fasili za dhana za msingi kama tafsiri, mfasiri, n.k

Ø  Tafsiri ni zoezi la kuhawilisha mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine.

Ø  Mfasiri ni mtu anayefanya kazi ya kutafsiri matini kutoka lugha moja hadi nyingine.

Ø  Fasili ni kufafanua maana ya neno kwa kina.

Ø  Ukalimani ni uhawilishaji wa mawazo yaliyo katika mazungumzo kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.

Ø  Mkalimani mtu anayefasiri papo kwa papo mazungumzo kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.

Ø  Lugha chanzi/chasili ni lugha iliyotumiwa katika matini chanzi

Ø  Lugha lengwa ni lugha inatumiwa katika matini lengwa.

Ø  Matini chanzi/ chasili matini inayotafisiriwa kwenda lugha nyingine

Ø  Matini lengwa ni matini iliyotafsiriwa katika lugha lengwa.

 

 

Mfasiri

Mfasiri ni mtu anayefanya tafsiri kutoka lugha moja hadi lugha nyinge. {TUKI:2000:165}

      Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, mfasiri ni mtu anayehamisha mawazo kutoka lugha moja (lugha chanzi) kwa kutumia lugha nyingine ili mawazo hayo yaeleweke na watu wasiojua au kuielewa lugha chanzi, na mawazo hayo sharti yawe katika maandishi.

Sababu za kuanzishwa kwa nadharia za tafsiri. Newmark (1982), Mwansoko na wenzake (2006) wanasema kuna mambo matatu yaliyosababisha kuanzishwa kwa nadharia ya tafsiri ambayo ni:-

           i) Wingi wa makosa katika tafsiri zilizochapishwa awali; ilionekana kwamba, kulikuwa na makosa mbalimbali kama vile makosa ya kimuundo, kimaumbo, kimsamiati nk. Pia ilikuwa ni nadra/muhali kupata tafsiri zisizokuwa na makosa.

            ii) Kuwepo kwa idadi kubwa (na inayoongezeka) ya asasi zinazojishughulisha na kazi za tafsiri. Hali hii ilisababisha kubuniwa kwa nadharia ya tafsiri ili kuwepo kwa misingi inayokubalika. Mfano; nchini

Tanzania peke yake kuna asasi nyingi zinazojishughulisha na tafsiri kama vile: BAKITA, TATAKI, SHIHATA, WAFASIRI na vyombombalimbali vya habari kwa mfano: TV, Magazeti nk.

           iii) Mfumuko wa istilahi katika taaluma mbalimbali hasa Sayansi na Teknolojia. Hivyo nadharia ya

tafsiri ilianzishwa kwa lengo la kuleta ulinganifu wa istilahi hizo kati ya lugha moja na nyingine ili

 

Umuhimu wa tafsiri/mfasiri

Tafsiri ina dhima zifuatazo:

§  Ni njia ya mawasiliano

§  Nyenzo ya kueneza utamaduni kutoka jamii moja hadi nyingine.

§  Mbinu ya kujifunza lugha za kigeni

§  Mbinu ya kukuza lugha

§  Mbinu ya kuhamisha maarifa na ujuzi

§  Njia ya kuongeza kipato{Kiuchumi}

2. Aina na mbinu za tafsiri

ü  Tafsiri ya neno kwa neno

           Hii ni tafsiri ambayo mofimu na maneno hufasiriwa yakiwa pwekepweke kwa kuzingatia maana zake za msingi bila kujali muktadha wala muundo wala utamaduni wa lugha lengwa. Mpangilio wa mofimu na maneno wa lugha chanzi haubadiliki,pia tafsiri hii hulenga tu kupata maana ya kimsingi au ya kamusi. Katika tafsiri hii matini iliyofasiriwa huandikwa chini ya matini ya

lugha chanzi. Mfano

                       a)     Kiingereza:  this is a scien - tific text

                             Kiswahili: hii ni Ø sayansi – ki matini

                        b)    Kiingereza: we will translate many more work - s

                              Kiswahili: tu – ta tafsiri n - ingi zaidi kazi – Ø

                        c) A – li – safiri kwa basi.

                            S /he |past| travel by bus.

Ambapo:  Alama  ya  sufuri,  Ø,  huashiria  kutokuwa  kwa  kisawe  kwa  vileumbo linganifu halitumiki katika lugha pokezi

 

ü  Tafsiri sisisi

Tafsiri hii hutoa maana za kimsingi za maneno yakiwa pwekepweke kwa kuzingatia kanuni za kisarufi za lugha lengwa hususani sintaksia. Mbinu hii haizingatii muktadha wala utamaduni wa lugha lengwa.

 

 

ü  Tafsiri ya Kisemantiki

Mbinu hii ya tafsiri hufasiri kila neno katika sentensi jinsi lilivyo lakini kwa kufuata sarufi ya lugha lengwa. Tafsiri ya kisemantiki huwekea mkazo kwenye maana ya matini kama ilivyokusudiwa na mwandishi.

ü  Tafsiri ya Kimawasiliano

Tafsiri hii inazingatia na kumlenga msomaji wa matini lengwa ambaye hatarajii kupata ugumu wowote katika matini anayosoma, anatarajia kupata tafsiri nyepesi ya dhana za kigeni katika utamaduni wa lugha yake.

 

 

3. Masuala ya kiutendaji katika tafsiri

 Dhima za lugha na aina za matini

Aina za matini za tafsiri

        i. Matini elezi (Expressive Texts);

Ni aina ya matini ambayo hujiegemeza zaidi kwa mwandishi, mwandishi anatumia lugha kuelezea hisia zake bila kujali ujumbe huo utapokelewa vipi na wasomaji. Mfano wa matini elezi ni kama: ushairi, hadithi fupi, tamthiliya, riwaya, hotuba,nyaraka za kisheria, wasifu nafsi, insha nk.

      ii. Matini arifu (informative Texts);

Hizi ni matini zinazohusu mada yoyote ile ya maarifa kama sayansi, teknolojia, biashara na uchumi. Matini hizi huwa zinaandikwa katika maumbo sanifu, mfano vitabu, ripoti za kiufundi, tasnifu au Makala katika magazeti ama majarida ya kitaaluma n.k

       iii. Matini amili (Persuasive Texts);

Ni aina ya matini ambayo imeegemea zaidi upande wa wasomaji. Matini amili zinalenga kuibua hisia za msomaji na kumfanya afikiri au atende kwa maana ambavyo imekusudiwa na matini mahususi. Mfano wa matini hizi ni matangazo, maombi mathalani ya kazi au kitu kingine, maelekezo, propaganda na mialiko.

       iv. Matini za kifasihi

Ni matini zinazohusu maandiko ya kifasihi kama hadithi fupi, riwaya, ushairi na tamthiliya

       v. Matini za kiasasi

Ni matini zinazohusu siasa, biashara, fedha, sheria, serikali na asasi nyinginezo.

       vi. Matini za kisayansi.

Ni matini zinazojumuisha Nyanja zote za sayansi na teknolojia. Mfano maelekezo ya matumizi ya vifaa mbalimbali vya kielektroniki.

       vii. Matini za kiufundi

Hizi ni matini zinazotumia kiwango kikubwa cha msamiati wa kitaalamu au istilahi. Mfano matini za utabibu, za kisheria na kisayansi.

        viii. Matini zisizo za kiufundi

Hizi ni matini zinazotumia msamiati wa kawaida, mfano hotuba za viongozi mbalimbali, kadi za mialiko n.k

 

 

Uchambuzi wa matini ya tafsiri

 Kabla ya  kutafsiri ni muhimu Kusoma matini nzima ili kubaini

v  Lengo la matini     

v   Lengo la mfasiri  

v  Wasomaji lengwa

v  Umbo la matini lengwa

v   Mtindo wa matini chanzi

v   Ubora na mamlaka ya matini chanzi

Mchakato wa kufasiri

          Hatua muhimu

                             (I)            Maandalizi

                           (II)             Uchambuzi

                         (III)            Uhawilishaji

                         (IV)            Usawidi wa rasimu ya kwanza ya tafsiri

                           (V)            Udurusu wa rasimu ya kwanza ya tafsiri

                         (VI)            Kusomwa kwa rasimu ya tafsiri na mtu wa pili

                       (VII)            Usawidi wa rasimu ya mwisho ya tafsiri

 

 

        i.            Maandalizi ya kutafsiri

Katika hatua hii, mfasiri anatakiwa kufahamu vizuri maudhui ya matini chanzi, ujumbe wake, mtindo wa matini na kuwekea alama sehemu zenye utata au zisizoeleweka vizuri, anashauriwa kupigia mstari au kuandika katika kidaftari kidogo msamiati, istilahi na misemo muhimu ya matini chanzi kama vile, methali, nahau maneno ya kitamaduni yasiyotafsirika, majina maalumu, n.k. kwa kupigia mstari au kuyaandika katika kidaftari kidogo ili iwe rahisi kwa mfasiri kuyatafutia visawe vyake kabla hata ya kuanza kutafsiri lakini pia kumsaidia mfasiri asiyasahau wakati wa kutafsiri au kuyatolea ufafanuzi zaidi katika tafsiri yake.

      ii.            Uchambuzi wa matini chanzi

Katika hatua hii, mfasiri anatakiwa kuchunguza kwa makini maneno, methali, nahau, misemo pamoja na maelezo mengine ya matini chanzi aliyoyaandika au kuyapigia mstari katika hatua ya maandalizi na kuyatafutia visawe vyake katika lugha lengwa, hapa mfasiri anashauriwa kutumia marejeo mbalimbali kama vile, kamusi, ensiklopedia, orodha ya msamiati na istilahi mpya. Mfasiri anatakiwa kuwa na shajara au daftari dogo kwa ajili ya kuandika na kuhifadhi maneno na maelezo muhimu ya matini chanzi na visawe vyake, visawe vinavyoonekana kufaa viorodheshwe vizuri ili iwe rahisi kuvirejelea wakati wa kutafsiri, vilevile mfasiri kama ataona kuwa matini chanzi ni ndefu sana, anashauriwa kuigawa matini hiyo katika sehemu ndogondogo kama vile, sura, aya au sentensi na kuanza kushughulikia sehemu moja baada ya nyingine.

    iii.            Uhawilishaji

Uhawilishaji ni uhamishaji wa mawazo kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa, au uhamishaji wa mawazo au ujumbe kutoka matini asilia kwenda matini ya tafsiri. Hii ina maana kuwa katika hatua hii, visawe vya kisemantiki [kimaana] vya matini chanzi vilivyobainishwa katika hatua ya uchambuzi huamishwa katika matini lengwa [kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa] na kupangwa vizuri kisarufi na kimantiki ili fasiri hiyo iwe na maana kwa wasomaji wake.

     iv.            Kusawidi /Kuandaa rasimu ya kwanza ya tafsiri.

Katika hatua hii, mfasiri huandika rasimu yake ya kwanza ili kupata picha fulani ya matini aliyoikusudia, katika uandaaji wa rasimu ya kwanza, kwa kufanya hivi, mfasiri anaweza kugundua kuwa anahitaji taarifa zaidi tofauti na alizozipata katika hatua ya uchambuzi, na hivyo kulazimika kuchunguza zaidi matini chanzi na hata kupekua zaidi na zaidi marejeo yake aliyoyaandaa kwa kuyatumia katika tafsiri. Jambo la kuzingatia, mfasiri anatakiwa wakati akihamisha mawazo au ujumbe azingatie umbo na lengo la matini chanzi ili kutoathiri tafsiri yake.

       v.            Kudurusu / kuipitia rasimu ya kwanza

Baada ya kusawidi rasimu ya kwanza, mfasiri anatakiwa kuivundika rasimu yake ya tafsiri kati ya juma moja hadi mawili baada ya kukamilika kwake na kuanza kuidurusu/ kuipitia rasimu hiyo kwa jicho la kihakiki zaidi na kuangalia kama kuna makosa ambayo yamejitokeza katika rasimu yake au la na kuyafanyia marekebisho pale inapobidi.

     vi.            Kusomwa kwa rasimu ya tafsiri na mtu/watu wengine

Baada ya mfasiri kuipitia rasimu yake ya kwanza, na kuifanyia masahihisho kwa makosa yaliyojitokeza, anatakiwa kuwapa watu wengine waidurusu rasimu hiyo iliyofanyiwa marekebisho ili waipitie tena na kuirekebisha, hivyo basi wasomaji hao wanaweza wakahakiki,wakashauri, n.k. Wasomaji hawa husaidia kuona kama tafsiri iko sahihi, inaeleweka na ina mtiririko mzuri wenye mantiki.

   vii.            Usawidi /Kuandika rasimu ya mwisho

Baada ya kupata maoni kutoka kwa wasomaji wa pili, mfasiri anaweza kuyatumia maoni, mapendekezo na maelekezo yao kusahihisha tena tafsiri yake na hatimaye kuandaa na kutoa rasimu ya mwisho ambayo itakuwa tayari kwa kusomwa na wasomaji.           

Baada ya kuangalia maana ya tafsiri, sasa tuangalie  sifa anazotakiwa kuwa nazo mfasiri:

Sifa za mfasiri bora

Mfasiri bora anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:

·         Awe na ujuzi wa lugha fasaha, hii ina maana kuwa awe anajua kwa ufasaha lugha zote mbili, yaani lugha chanzi na lugha lengwa. Hii ni kujua vizuri nyanja mbalimbali za Isimu ya lugha husika kama vile; Fonolojia-{Matamshi}, Mofolojia-{Maumbo}, Sintaksia-{Muundo} na Semantiki-{Maana}

·         Awe na ufahamu mkamilifu wa ujumbe au mada iliyoandikwa katika matini chanzi na uwezo au jinsi ya kuelezea ujumbe au mada hiyo kwa ufasaha katika lugha lengwa.

·          Awe amesoma  maandishi ya matini chanzi hadi ayafahamu kinaga ubaga halafu aweze kuyafikiria katika lugha lengwa.

·         Aweze kutambua  tamaduni za lugha chanzi na lugha lengwa.

·         Aweze kuibua hisia sawa kwa walengwa kama ilivyo katika matini chasili

·         Awe na stadi za uhakiki matini.

·         Awe na tajiriba kubwa ya usomaji wa aina mbalimbali za tafsiri.

·          Awe na tabia yakushirikiana na watu wengine katika shughuli za kufasiri.

4. Matatizo yanayojitokeza katika tafsiri

Ø  Matatizo ya kitamaduni

Mfasiri daima hulenga kuhawilisha maana kwa mujibu wa utamaduni wa jamii husika hivyo lugha zenye utofauti sana kiutamaduni huwa tatizo kwa mfasiri.

Ø  Matatizo ya kiisimu

Tatizo hili hujitokeza iwapo mfasiri anafasiri lugha mbili zinazotengana sana kiisimu.

Ø  Matatizo ya kimtindo

Yampasa mfasiri kuuelewa upekee wa mwandishi,wakati mwingine mfasiri anapojitahidi sana kuhifadhi mtindo wa mwandishi huishia kutoa tafsiri tenge.

Ø  Uundaji wa maneno mapya

Hali hii hutokea iwapo mfasiri anapokosa kabisa visawe vya istilahi za lugha chanzi katika lugha lengwa.

Ø  Matatizo ya kiitikadi

 

(i)..Tofauti za kiisimu kati ya lugha chanzi na lugha lengwa. Tofautui za maumbo, miundo na maana kati ya lugha ya Kiswahili na lugha ya Kingereza wakati mwingine husababisha matatizo au upungufu katika tafsiri na ukalimani. Kwa mfano maumbo ya vitenzi vya Kiingereza huruhusu kauli nyingi elekezi kutoonesha umoja au wingi wa wahusika wala majina ya vitu mahususi vinavyoambatana na maelekezo yanayotolewa tofauti maumbo ya vitenzi vya Kiswahili ambavyo huonesha umoja na wingi wa wahusika na hata kuwa na majina ya vitu husika, tazama mifano ifuatayo kama ilivyotolewa na, Mwansoko [2006]

Kingereza__ Kiswahili

No parking? Usiegeshe gari hapa [je kisichoruhusiwa kuegeshwa ni gari tu?]

No Smoking? Usivute sigara[ Je ni sigara tu ndiyo hairuhusiwi kuvutwa?]

Arrivals? Wanaowasili

Departures? Wanaosafiri

Vilevile tofauti za maana kati ya lugha ya Kingereza na Kiswahili huweza kuathiri tafsiri au ukalimani, mathalani: 

              Kiswahili__ Kingereza

Wasiojiweza? Disabled [Siyo wote wasiojiweza ni walemavu]

[na siyo walemavu wote hawajiwezi]

Wezi wa mifukoni? Pickpockets [Hawaibi kwenye mifuko, wanaiba kutoka

Mifukoni]

(ii) Tofauti za mitindo kati lugha chanzi na lugha lengwa

             Tofauti za mitindo ya uzungumzaji pia, huweza kuathiri tafsiri na ukalimani na hii ni kwa sababu unaweza kukuta kuna mitindo fulani inaweza kutumika katika muktadha fulani lakini ikishindwa kupata tafsiri katika lugha nyinginekatika muktadha ule ule mathalani:

Kingereza: Kiswahili

(i) Thou shalt not steal [mtindo wa kidini] Usiibe. Do not steal [mtindo wa kawaida]  Usiibe

(ii) Lend me your ears [mtindo wa kishairi]  Naomba mnisikilize May I have your attention [kawaida]  Naomba mnisikilize

Tafsiri zote tulizoziangalia katika mfano wa (i) na (ii) zimetoa maana au taarifa ili ile iliyomo katika matini chanzi lakini tafsiri hizo hazikuzingatia mtindo wa lugha iliyotumika katika matini chanzi.

(iii) Tofauti za kitamaduni kati ya lugha chanzi na lugha lengwa

Tofauti za kiutamaduni, yaani taofauti za kimila, desturi na mazingira ya watumiaji wa lugha chanzi na lugha lengwa huweza kufanya tafsiri au ukalimani kuwa mgumu, kwa mfano, katika utamaduni wa Waingereza wana milo minne wakati Waswahili wana milo mitatu na hii hupelekea kuwa

vigumu kupata dhana za milo ya hiyo ya Waingereza katika dhana ya Kiswahili. Mfano:

 

  Waingereza wana: Waswahili wana:

Breakfast ------------------ Kifungua kinywa

Lunch …………………... Chakula cha mchana

High tea ……………………?

Dinner ……………………Chakula cha jioni

Supper …………………….?

Kwa hiyo ukiangalia mifano hiyo, utaona kuwa, high tea na supper kuzipata dhana zake katika lugha ya Kiswahili ni ngumu kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kuwa na milo kama hiyo kwa siku. Lakini pia inakuwa vigumu kupata tafsiri ya vyakula kama vile ugali, makande katika lugha ya Kiingereza kutokana na kutokuwa na vyakula vya aina hiyo.

(iv) Tofauti za kiitikadi kati ya lugha chanzi na lugha lengwa

Tofauti za kiitikadi pia huweza kuathiri tafsiri na ukalimani, na hii ni kwasababu, utakuta wafasiri wengi hususani waandishi wa habari kuegemea katika itikadi zaidi, kwa mfano:

      Kingereza Kiswahili

Bussnessman ? mlanguzi [tafsiri hii inatokana mfasiri kuathiriwa na itikadi ya ujamaa] mfanyabiashara [tafsiri hii inatokana mfasiri kuathiriwa na itikadi ya ubepari]

Freedom fighter ? wapigania uhuru [Tafsiri ya vyombo vya habari vya Tanzania wakati wa kupigania uhuru] Magaidi [Tafsiri ya idhaa ya BBC na Radio za Afrika

Kusini wakati huo]

Hivyo basi

5. Aina za tafsiri.


*      Tafsiri ya fasihi

§  Tafsiri ya riwaya

§  Tafsiri ya tamthiliya

§  Tafsiri ya ushairi

§  Tofauti ya tafsiri za kifasihi na zisizo za kifasihi.

 

 

©  Tafsiri ya matini za kisayansi/ kiufundi

      Matini za kisayansi au za kiufundi ni zile matini zinazotumia msamiati maalum, mfano matini za tiba, uhandisi, elektroniki, sayansi ya kompyuta na sayansi nyinginezo. Tafsiri ya matini hizi haijiegemezi katika utamaduni wowote na hutofautiana na tafsiri nyingine kutokana na matumizi makubwa ya istilahi. Matini za kiufundi pia hutumia picha, grafu, michoro, vielelezo, takwimu n.k na huandikwa katika umbo la ripoti ya kiufundi. Mfasiri anapofasiri matini hizi hukumbana na zoezi la uundaji wa istilahi mpyakutokana na kukosa visawe vya istilahi za lugha chanzi katika lugha lengwa.

©  Tafsiri na Utamaduni

      Lugha ni kipengele cha utamaduni wa jamii, pia lugha inatumika kuelezea utamaduni wa jamii husika. Maana za maneno katika lugha hujengwa kutokana na utamaduni wa jamii inamozungumzwa lugha hiyo. Hivyo tafsiri siyo tu mchakato wa kiisimu, bali pia ni mchakato unaojumuisha masuala yanayohusu utamaduni wa wazungumzaji wa lugha husika. Tofauti za kiutamaduni baina ya lugha chanzi na lugha lengwa ndizo zinampatia mfasiri matatizo makubwa

wakati wa kufasiri, mathalani mfasiri anapofasiri lugha ya Kiingereza na lugha ya Kiswahili. Vipengele vya kiutamaduni vinavyoweza kuleta ugumu katika kufasiri ni kama nguo, vinywaji, violwa, ekolojia, siasa na dini.

©  Tafsiri ya mashine na tafsiri ya binadamu

     Mchakato wa kufasiri huweza kufanywa na binadamu au mashine. Mchakato wa kufasiri kwa kutumia mashine umekuja kutokana na maendeleo ya sayansi na tekonolojia ambapo badala ya binadamu kutumia maarifa yake zipo mashine ambazo zinaweza kufanya kazi hiyo.

 

6.Tafsiri na ukalimani

Tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine. Ukalimani ni uhawilishaji wa ujumbe au mawazo ulioko katika mazungumzo kutoka lugha moja hadi nyingine. Hizi ni taaluma zenye uhusiano kwani zote zinahusika na kuhawilisha ujumbe au mawazo kutoka lugha moja hadi nyingine.

 

Katika ukalimani matini chanzi huwa katika mazungumzo na matini lengwa pia huwa katika mazungumzo. Katika ukalimani mkalimani hana muda wa kutosha wa kujiandaa kwa sababu anatakiwa kukalimani kile anachosikia wakati ambapo mzungumzaji anaendelea kuzungumza mambo mengine.

Aina za ukalimani

Kuna aina mbalimbali za ukalimani kutegemeana na vigezo unavyotumia kuainisha au kupata hizo aina;

1. Kigezo cha kwanza ni kigezo cha Muktadha; Katika kigezo hiki vipengele vinavyojitokeza ndani ya muktadha ili kupata aina tunazingatia mahali, lengo, aina ya hadhi, sifa za walengwa nk.

©  Ukalimani wa Kijamii/community interpretation:

Huu ni ukalimani ambao hufanywa katika masuala mbalimbali ya kijamii kama vile afya, ujenzi wa shule huduma za kijamii kama vile maji, umeme, masuala ya mihadhara ya kidini nk.

©  Ukalimani wa Mikutano au Makongamano/Conference;

Huu ni ukalimani unaofanyika katika makongamano au mikutano

mbalimbali. Mara nyingi aina hii ya ukalimani inafanyika katika mikutano ya kimataifa.

©  Ukalimani wa Mahakama/Mahakamani;

Aina hii hufanywa na wanasheria katika mahakama za ngazi mbalimbali. Pia huitwa ukalimani wa kisheria.

©  Ukalimani wa Kitabibu; Huu ni ukalimani ambao unafanyika mahali ambapo matibabu yanapatikana, kwa kiasi kikubwa aina hii ya ukalimani inafanyika katika hospitali kubwa kubwa.

©  Ukalimani wa Habari/katika vyombo vya habari; Huu ni ukalimani unaofanywa katika vyombo mbalimbali vya habari, hususani redio na televisheni ili kuiwezesha hadhira lengwa iweze nayo kuelewa matangazo yanayotolewa kwa lugha chanzi.

©  Ukalimani Sindikizi/Escort interpretation; Katika aina hii ya ukalimani mkalimani hufuatana na mtu au kikundi cha watu katika safari au katika usaili au mahojiano.

2. Kigezo cha pili ni kigezo cha Muundo au Mfumo wa Lugha/Language mode/modality; Katika kigezo hiki lugha inayotumika katika ukalimani inaweza ikawa lugha ya kusema/kizungumza na lugha ya alama. Kupitia lugha ya alama tunapata aina moja ya ukalimani yaani ukalimani wa viziwi

Kwa kupitia lugha ya mazungumzo au kusema tunapata aina mbili za ukalimani ambazo ni;


*      Ukalimani Mfululizo/Andamizi/Simultaneous interpretation; Katika ukalimani mfululizo, kama jina lenyewe linavyodokeza mkalimani huzungumza takribani sambamba na mzungumzaji wa lugha chanzi. Katika aina hii ya ukalimani mkalimani lazima afanyekazi kwa haraka

sana ili kuendana na kasi ya mzungumzaji kuepuka kupitwa na mambo muhimu.

Katika ukalimani mfululizo makalimani huketi katika chumba maalum cha ukalimani (booth) ambacho hakipitishi sauti (sound proof) na kisha huzungumza kwa kutumia kipaza sauti huku akimwona na kumsikia mzungumzaji wa lugha chanzi kupitia visikizio (ear phones)


*      Ukalimani Fuatishi/Mtawalia (Consecutive interpretation); Katika ukalimani fuatishi mkalimani huzungumza/hukalimani baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kumaliza ujumbe wake au hata kama hajamaliza ujumbe wake baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kutulia kwa sekunde kadhaa ili kumpa makalimani fursa ya kukalimani kile kilichosemwa. Katika aina hii mkalimani na

mzungumzaji wa lugha chanzi mara nyingi wanakuwa pamoja wakiwa wamesimama kwenye jukwaa au wakiwa wameketi mezani.

 

Sifa za Mkalimani

a)      Awe na ujuzi wa hali ya juu wa lugha anazoshughulika nazo pamoja na utamaduni wake.

b)      Ajue lugha zaidi ya mbili za kimataifa kwani kadiri unavyojua lugha zaidi ndivyo unavyokuwa   mkalimani bora zaidi.

c)       Awe na ujuzi au maarifa ya kutosha juu ya mada, taaluma au uwanja unaozungumziwa. Inamaana kwamba kama wewe ni mkalimani wa masuala ya kiuchumi basi hupaswi kufasili masuala ya kisheria. Mfano; ukalimani wa mahakamani hufanywa na wanasheria.

d)      Awe na ujuzi wa taaluma ya ukalimani; yaani awe amepata mafunzo ya ukalimani. Katika hayo mafunzo atajifunza mbinu za ukalimani aina, changamoto na namna ya kuzikabili.

e)      Awe na kipaji, yaani; Uwezo wa kukumbuka, Kuteua msamiati sahihi kwa haraka, Kipaji katika kuunda istilahi haraka haraka na kuitumia. Kipaji cha ulumbi/awe na ulumbi yaani kipaji cha kuongea na kuvuta watu. (eloquency)

 

                                        Mfano wa Tafsiri

                                                        Kiingereza                                                          Kiswahili

                                           vision                                                  >             ono

                                             six                                                      >             sita (thenashara)

around me                                        >             kunizingira

suffused                                              >             jaa

clear light                                           >             mwanga safia

fine mid-summer morning        >             asubuhi nadhifu ya kiangazi

dim light                                            >             mwanga hafifu

wet dawn                                           >             mapambazuko nyevunyevu

May                                                       >             mwezi wa Mei

warning                                               >             onyo? ishara awali?

gold lettering                                   >             herufi zilizonakishiwa dhahabu

glow                                                     >             angaza? nawiri?

 

 

         Uwakilishi huu unamulika ugumu wa kupata visawe. Unapokosa visawe, unatafsiri kwa

kufasiri au kufafanua maana. Mbinu hizi zimetumika kwa matini za without warning’ >

bila  ishara  awali,  na,  gold  lettering’  >  herufi  zilizonakishiwa  dhahabu,  mtawalia.

Kulingana na matumizi ya lugha unayokabili, ni muhimu kuzingatia masharti yafuatayo:

Majina maalumu hayatafsiriwi, isipokuwa pale pana tafsiri au neno-mkopo tayari.

Zingatia neno Biblia.

Majina  ya  mashirika  au  nyadhifa  huwakilishwa  kwa  tafsiri  sisisi,  kama  vile Redcross>Msalabamwekundu au Chairperson > Mwenyekiti. Semi za lugha hutafutiwa visawe katika katika lugha pokezi. Zingatia: ‘One rotten

apple spoils the whole barre.’l >Nazi mbovu harabu ya nzima. Kisawe kikikosa, unawakilisha ujumbe kwa usemi linganifu au tafsili ya maana. Mara kwa mara, unaruhusiwa kukopa sisisi hasa ukijikuta umekwama kabisa na maendelezo ya neno yawe hayakaidi kanuni za mfumo wa sauti wa lugha pokezi. Maneno mora, data, ajenda ni mifano mizuri ya mikopo sisisi.

 

Mifano ya matini zilizotafsiriwa

                       Matini ya habari

 Matini Chasili: Kiingereza

                          The  Secretary  General  of  the  United  Nations  Organization,  Kofi  Annan,  fired  one  top

                           official blaming him for failing to ensure the security of the officers of the organization.

                           Mr.  Annan  also  chastised  a  highly  respected  deputy,  Ms.  Louise  Frechette  of  Canada,

                          who submitted her resignation but Mr. Annan refused to accept it. The action yesterday

                           appeared to be unprecedented in the United Nations Organization, where senior officers

                            are almost never rebuked publicly for such an offence.

 

 Matini Tafsiri: Kiswahili

                           Katibu  Mkuu  wa  Umoja  wa  Mataifa,  Kofi  Annan,  alimwachisha  kazi  kinara  wake  wa

                           usalama  akimlaumu  kwa  kushindwa  kuhakikisha  usalama  wa  maafisa  wa  umoja  huo.

                           Annan pia alimshutumu vikali naibu wake, Bi. Louise Frechette wa Canda, lakini alikataa

                           ombi lake la kujiuzulu. Hii ni mara ya kwanza kinara wa umoja huo kuzomea waziwazi

                            maafisa wake kwa kufuatia kosa kama hilo.

Tafsiri  hii  imehamisha  ujumbe  muhimu  lakini  ikashindwa  kuhifadhi  maana  kamilifu.

Baadhi ya maana huonekana kupotea na zingine kupotoshwa. Tunabaini upungufu huu kwa kulinganisha baadhi ya kauli za matini hizi:

 

 

                                        Kiingereza                                                        Kiswahili

                                     one top official                                       kinara wake wa usalama

                                      a highly respected deputy              naibu wake

                                     submitted resignation?

                                      appeared unprecedented                 ndio mara ya kwanza kinara . . .

                                      publicly                                                    waziwazi

 


Kwanza kabisa, maana katika ‘submitted resignation’, haionekani kushughulikiwa. Arifa katika kauli hii imetolewa kwa maana ya kushadidia uzito wa kitendo cha Katibu Mkuu wa Muungano wa Mataifa. Pili, maana za kauli zingine zimepotoshwa ifuatavyo: Kauli  ya  ‘One  top  official’  haina  maana  ya  kinara  wa  usalama.  Fasiri  hii imekiuka mipaka ya maana    matini na kupotosha ujumbe. Maana ya ‘highly respected’ haikushughulikiwa. Tena, matumizi ya kibainishi, {a}, ina maana ya kuwa kuna manaibu wengine, na si yule mmoja pekee. Kauli ya ‘appeared unprecedented’ Ina maana ya kuwezekana kuwa mwanzo, na sio kuwa kwa uhakika unaosikika katika kauli “hii ndio’’. Neno publicly halina maana ya “waziwazi” ila hadharani. Tendo linaweza kuwa waziwazi lakini pia faraghani.

 

Matini ya riwaya

Matini Chasili: Kiingereza

             The car sped smoothly along the coast road.  Its own smooth running mixed with the soft Sounds of the sea flowing over the sands.  The  man  closed  his  eyes,  and  like  a  piece  of twine, the thought run round and round his head that it would never be possible to look at such comfortable things and feel real contempt for them. Envy, certainly, but not contempt.

 

 

Matini Tafsiri: Kiswahili

         Gari  ilishika  kasi  ilipofika  ile  barabara  iliyoko  karibu  na  pwani.  Ile  sauti  tulivu  ya  mngurumo  wa

hiyo gari ilichanganyika na sauti ya bahari inayofurikia michangani. Yule bwana alifunga macho na humo  ubongoni  mwake  akawa  anazungukwa  na  fikira  kwamba  haitawezekana  kabisa  kuviangalia vitu vizuri namna ile kisha ukavidharau. Kuingiwa na husuda au kijicho ndio; lakini si dharau.

 

Matini chasili inatafakari vile tajiriba zetu za maisha ya anasa na starehe huja kuathiri mielekeo yetu. Ujumbe huu umehifadhiwa katika matini tafsiri, licha ya hitilafu wazi za baadhi ya maana. Hitilafu hizo zajitokeza kulingana na tafsiri za kauli kama:

                                    

                                       Kiingereza          Kiswahili

                                   sped smoothly                     ilishika kasi

                                                      coast road            barabara iliyokaribu na pwani                                  

                               smooth running         sauti tulivu

                                             comfortable things                     vitu vizuri

                           env  like a piece of twine   ?      husuda au kijicho

Hitilafu hizi huashiria upotovu au upungufu wa maana unaoweza kufafanuliwa ifuatavyo:

Kauli  ya  ‘speed  smoothly’  yaashiria  mwendo  wa  utulivu.  Kuna  shaka  kama kushika kasi kuna maana ya utulivu. Mara nyingi huwa ni kinyume chake.

Kauli ya ‘smooth running’ hairejei mngurumo wa gari pekee. Tafsiri ya sauti tulivu, kwa hivyo, imebana maaana ya Kiingereza. ‘Coast road’ si lazima iwe ni ile barabara iliyo karibu na pwani. Inaweza kuwa ni barabara ya kuelekea pwani: barabara ya pwani.

 

 

 Matini ya Kishairi

Shairi ni tungo linalotiririsha taswira, mawazo na ujumbe kwa lugha nzito ya mkato, yenye mnato wa maana. Umbo la shairi hurejelea idadi ya beti zake. Hata hivyo, kila ubeti unafaa kuwasilisha ujumbe kamilifu unaowiana na maana ya shairi nzima. Ubeti mfupi ufuatao kutoka, Wimbo wa Lawino, ni mfano wa tafsiri ya shairi. Umenukuliwa kutoka Mwansoko (1996).

Matini Chasili: Kiingereza                                          Matini Tafsiri: Kiswahili

Maria the clean woman                                     “Maria Mtakatifu

Mother of the Hunchback                                  Mama wa Mungu

Pray for us                                                             Utuombee

Who spoil things                                                 Sisi wakosefu

Full of Graciya.”                                                   Uliyejaa neema.”

 

            Matini chasili ni kinaya na imetumia lugha ya mzaha kimakusudi. Mtunzi wa ubeti huu                analenga kukejeli imani na mafunzo ya Kikatoliki. Matini tafsiri imepuuza dhamira hii na adala yake ikatumia lugha ya kawaida ya heshima na uungwana. Kwa kufanya hivi,  tafsiri imeikaidi dhamira na mwelekeo wa mwandishi wa matini chasili.

 

 

 

Mifano ya tafsiri ya kimawasiliano:

Tanzania National Electric Supply Company Limited.        > Shirika la umemeTanzania.

A bird in the hand is worth two in the bush.                       > Fimbo ya mbali haiui nyoka.

A burnt child dreads fire.                                                         > Mtoto akililia wembe, mpe.

Actions speak louder than words                                          >Ada ya mja hunena, mwungwana ni kitendo.

A drowning man will catch at a straw.                                  >Mfa maji haachi kutapatapa.

All good things come to those who wait.                             > Subira huvuta heri.

A stitch in time saves nine.                                                      >Usipoziba ufa utajenga ukuta.

As you sow, so you shall reap                                                 >Upandavyo ndivyo uvunavyo

Charity begins at home                                                            >Kutoa ni moyo si utajiri.

Clothes don’t make the man.                                                  > Usichague mchumba siku ya Idi.

Mtoto wa nyoka ni nyoka.                                                        >Like father like son

     Kwa hiyo mfasiri yeyote yule ni muhimu kuteua mbinu atakayotumia wakati wa kutafsiri kulingana aina ya matini anayotaka kutafsiri. Hata hivyo ni vigumu kutumia mbinu moja pekee katika kutafsiri, kwani mbinu zote huweza kujitokeze katika tafsiri kwa mfano, maneno mengine huweza kufasiriwa kisisi au kisemantiki lakini pia ni lazima iwepo mbini ambayo inatawala mbinu zote. Wataalam wengi wa tafsiri wanapendekeza mbinu ya tafsiri ya kimawasiliano itumike zaidi hususani katika matini zenye lengo la kuelimisha au kuleta athari sawa na ile ile iliyopo katika matini chanzi. Matini kama vile za kisheria mbinu muafaka zaidi ni ile ya kisemantiki.

 

Zoezi

1. Linganisha na linganua kati ya taaluma ya tafsiri na ukalimani.

2. (a) Tafsiri sentensi zifuatazo kwenda lugha ya Kiingereza

(i) Dua la kuku halimpati mwewe

(ii) Bandu bandu humaliza gogo

(iii) La kuvunda halina ubani

(iv) Mla vya watu naye vyake huliwa

(v) Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli

(b) Ni njia gani umetumia katika tafsiri ulizotoa hapo juu, unadhani ni kwa nini?

3.Kwa kutumia mifano, fafanua istilahi zifuatazo:

[a] [i] Matini chanzi

     [ii] Matini lengwa

     [iii] Lugha chanzi

      [iv] Lugha lengwa

[b] Tafsiri sentensi zifuatazo kwenda lugha ya Kiswahili

(i) All that glister is not gold

(ii) Looser casn't be a chooser

(iii) When you make your bed you must lie on it

(iv) There is no incense for something rotting

(v) When in Rome do, do as Romans do

(vi) Do not pray for an easy life,pray for the strength to endure a difficult one.

(vii) Study without desire spoils the memory, and it retains nothing that it takes it.

(c) Ni njia gani umetumia katika tafsiri hizo ulizotoa hapo juu, unadhani ni kwanini?

4. "Mfasiri au mkalimani hukabiliana na changamoto mbalimbali katika kufanikisha kazi yake."   Huku ukitumia mifano thibitisha kauli hiyo.

 

 

 



A.Florence
 

Matini hii imeandaliwa na;

 

 

 

   ©2014                                                                                                                

 

“Elimu ni kile kinachobaki baada ya mtu  kusahau yale yote aliyojifunza shuleni”

 

 


antagonf@hotmail.com

 

Marejeo

Cartford, J. C. (1965). A Linguistic Theory of Translation. London: OUP.

Mwansoko, H.J.M. (1996) Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu, Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.

Newmark, P. (2003) A Textbook of Translation, England: Pearson Education Limited.

TUKI (2002). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar-es-salaam

Wanjala, S.F (2011) Misingi ya ukalimani na tafsiri, Se

Comments

Popular posts from this blog

MATOKEO YA MTIHANI WA DARASA LA SABA 2015 YOTE HAYA HAPA

Angalia yote hapa NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA PSLE-2015 EXAMINATION RESULT ARUSHA DAR ES SALAAM DODOMA IRINGA KAGERA KIGOMA KILIMANJARO LINDI MARA MBEYA MOROGORO MTWARA MWANZA PWANI RUKWA RUVUMA SHINYANGA SINGIDA TABORA TANGA MANYARA GEITA KATAVI NJOMBE SIMIYU   

HUYU NDIE MWANAUME"[SHOGA] MWENYE MAKALIO MAKUBWA KULIKO WOTE DUNIANI,KAAMUA KUPOST HIZI PICHA INSTAGRAM.

Kutana na mwanaume mwenye makalio makubwa kama mwanamke.Kwa jina anaitwa Micah,ni mwanaume ambaye hipsi na makalio yake zinazidi hata zile za wanawake huwezi kuamini hebu tazama hapa utakubali tu mwenyewe.

Matokeo ya kidato cha pili mwaka 2015: Zanzibar

MATOKEO YA MITIHANI YA KIDATO CHA PILI KWA MWAKA 2015 KIWILAYA MJINI MAGHARIBI KUSINI UNGUJA KATI KASKAZINI "A" KASKAZINI "B" MKOANI CHAKE CHAKE WETE MICHEWENI SKULI ZA BINAFSI TANBIHI: KWA UFAFANUZI WA SUALA LOLOTE LINALOHUSU MATOKEO YA MITIHANI TAFADHALI WASILIANA NA OFISI ZA BARAZA LA MITIHANI ZANZIBAR UNGUJA NA PEMBA - AHSANTENI. Source:    Ministry of Education and Vocational Training - Zanzibar Angalia Matikeo ya kidato cha pili bara hapa chini Posted by Maarifa & FIKRA Yakinifu on  Friday, January 15, 2016