MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Azam ilivuta sharubu za Simba baada ya kuilazimisha sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa ligi uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi.
Timu hizo ziliingia uwanjani zikiwa na kumbukumbu ya ushindi kwenye mechi zilizopita, Simba iliichapa Ndanda mabao 2-0, huku Azam ikiichabanga Kagera Sugar mabao 3-1.
Licha ya Simba kupata bao la mapema dakika ya 18 lililofungwa na Emmanuel Okwi, aliyetumia makosa ya kipa wa Azam, Mwadini Ally, Azam ndio walioanza kwa kasi ambapo dakika ya 12 kiungo, Frank Domayo, nusura aipatie bao timu hiyo baada ya kupiga shuti lililomlenga kipa wa Simba, Peter Manyika, aliyelidaka vema.
Bao alilofungwa Mwadini lilitokana na uzembe wake alioufanya wa kukaa vibaya langoni, hali iliyomfanya Okwi kumchungulia na kupiga krosi ya juu kuelekea langoni akiwa pembeni mwa uwanja na mpira kugonga mwamba wa juu na kujaa wavuni.
Dakika ya 28 winga wa Azam, Kipre Tchetche, nusura aipatie bao la kusawazisha timu yake akiwa ndani ya eneo la 18, lakini shuti alilopiga liliokolewa vema kwenye mstari na nahodha wa Simba, Hassan Isihaka.
Azam ilionekana kuutawala mchezo huo kwa vipindi vyote, licha ya Simba kutangulia kufunga bao lao, lakini juhudi zao za kutaka kusawazisha bao hilo zilishindwa kuzaa matunda hadi kipindi cha kwanza kilipomalizika.
Simba ilikianza kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko kwenye eneo lake la ushambuliaji, ambapo kocha wake, Goran Kopunovic, alimtoa Elias Maguli, aliyeonekana kupwaya na nafasi yake kuchukuliwa na Mganda, Simon Sserunkuma.
Kocha wa Azam, Joseph Omog, dakika moja baadaye naye alimpumzisha kiungo wake, Frank Domayo na kuingia winga, Khamis Mcha ‘Vialli’.
Mabadiliko hayo yalionekana kuineemesha Azam ambayo ilianza kufanya mashambulizi mfululizo kwenye lango la Simba, ambapo makosa yaliyofanywa na beki, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, aliyeokoa mpira vibaya dakika ya 57 yalimpa mwanya Tchetche aliyefanikiwa kuisawazishia timu yake baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Simba, Manyika Peter.
Simba ilifanya mabadiliko tena dakika ya 60 kwa kumtoa Okwi aliyeumia baada ya kugongana na beki wa Azam, Aggrey Morris, nafasi yake ilichukuliwa na kiungo, Awadh Juma. Baada ya kutolewa Okwi alipelekwa moja kwa moja vyumbani kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Dakika chache baadaye mwamuzi wa mchezo huo, Kennedy Mapunda, alimwonyesha kadi ya njano Mcha baada ya kumfanyia madhambi Jjuuko Murshid.
Azam itajilaumu yenyewe kwenye mchezo huo baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi kupitiwa kwa washambuliaji wake Mcha, John Bocco na Didier Kavumbagu, kwani hadi dakika 90 zilipomalizika timu hizo zilitoshana nguvu kwa sare hiyo.
Kwa matokeo hayo wachezaji wa Simba wameshindwa kupata donge nono la Sh milioni 10, waliloahidiwa kupewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo, Zacharia Hans Poppe, kama wangeifunga Azam.
Hata hivyo, taarifa zilizolifikia MTANZANIA wakati likienda mitamboni zilieleza kuwa Okwi amelazimika kukimbizwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili kupata matibabu zaidi kufuatia maumivu ya shingo aliyoyapata baada ya kugongana na Morris.
Okwi aliyekuwa amepoteza fahamu kufuatia kugongana na beki huyo wa Azam, alikimbizwa hospitali baada ya kupatiwa huduma ya kwanza hadi fahamu zilipomrejea na kudai aligongwa vibaya kwenye eneo la shingo yake.
Matokeo mengine kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, watani wa jadi wa mkoa huo, Mbeya City waliweza kutoshana nguvu kwa sare ya mabao 2-2. Mabao ya Mbeya City yalifungwa na Paul Nonga na Themi Felix, huku Prisons ikipata mabao yake kupitia Boniface Hau na Lugano Mwangama.
Mtibwa Sugar ambayo ilikuwa timu pekee ambayo haijafungwa mpaka sasa kwenye mechi zake za ligi, jana iliangukia pua katika mechi yake ya 10 baada ya kufungwa mabao 2-1 na Ruvu Shooting mchezo uliofanyika Uwanja wa Mabatini, Pwani.
Ndanda FC nayo iliifunga Kagera Sugar mabao 2-0 mechi iliyofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, huku Coastal Union ikipata ushindi wake wa kwanza toka ianze kunolewa na Mkenya James Nandwa pale walipoichapa Stand United bao 1-0.
Comments
Post a Comment