Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ambaye ni Katibu Mwenezi wa Chama cha NCCR-Mageuzi, amesema hana sababu yoyote ya kuhama chama chake na kujiunga na chama kipya cha siasa cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania).
Kafulila alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali kuhusu kusambaa kwa tetesi katika mitandao ya kijamii kwamba, anahamia chama hicho akiambatana na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe aliyehamia chama hicho hivi karibuni.
“Tetesi hizo zinatokana na tabia yangu ya kuwa na marafiki wengi katika chama hicho kipya, lakini nashangaa nina marafiki wengi CCM na hata Chadema, lakini hawasemi nahamia vyama hivyo ila ACT. Hizo ni tetesi tu sina sababu ya kuhama chama changu,”alisema.
Alisema Zitto alihama Chadema kutokana na mgogoro uliokuwepo baina yake na Chadema, hivyo alikuwa na sababu ila yeye akihama bila kuwa na sababu, itakuwa haina maana.
Alisema yeye bado ni Katibu Mwenezi wa NCCR-Mageuzi na anaendelea na kampeni za kujenga chama hicho ikiwemo yeye kurudi bungeni pamoja na chama hicho kuongeza wabunge wengi zaidi.
Comments
Post a Comment