Waziri
wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira amewashambulia
watangaza nia wenzake kwa madai kuwa wanatumia pesa kusaka
uongozi.
Alisema
Tanzania inapita katika msimu mgumu kisiasa kutokana na baadhi ya watu
kutumia mabilioni ya fedha kusaka uongozi wa nchi, wakati uongozi si
biashara.
Wasira
alitoa kauli hiyo jana wakati akiwashukuru wanachama wa CCM
waliojitokeza kumdhamini katika Uwanja wa CCM Kirumba, kama sehemu ya
utaratibu wa chama hicho kuelekea mchakato wa kumpata mgombea urais
katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
“Jamani wakati wa kujaza watu kwenye viwanja bado haujafika, mikutano ya hadhara bado. Kwa hiyo si kwamba hatuwezi kujaza watu, tukitaka tunaweza, lakini wakati bado, utafika tutajaza watu.
“CCM
na taifa kwa sasa vipo katika mazingira magumu kisiasa, rushwa sasa
inainyemelea kwa kasi kubwa siasa, hii ni hatari sana, kamwe tusije
kubali nchi yetu kuwekwa rehani na kundi la mafisadi.
“Mtu
ambaye anataka kuiweka rehani nchi kamwe hawezi kuwa na hoja, ndio
sababu mmeanza kuona watu wanaishiwa hoja. Mtanzania yoyote yule
anayetumia mabilioni kununua nchi mwisho wa siku ataiuza tu,”alisema Wasira huku wadhamini wake wakishangilia.
Wasira alisema tatizo la rushwa katika siasa ni kubwa kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu kuamini kuwa wanaweza kuinunua CCM.
“Hivi
nani kakutuma kuinunua CCM? Unainunua kwa niaba ya nani. Nchi yetu
haipo sokoni, na wala hatujawahi kutangaza tenda ya kuuza nchi, sasa
mabilioni kwenye siasa ya kazi gani?” alihoji.
Aliwasihi Watanzania kuwa makini kwa sababu kuna kila dalili nchi inapelekwa sokoni na watu wachache wasio itakia mema.
Kada
huyo mkongwe wa CCM aliwataka Watanzania kujiuliza na kutafakari ni
wapi mabilioni yanayotumika yanatoka, na kuongeza kuwa wanaotoa fedha
hizo uwezo wao kifedha hauonekani katika kulipa kodi.
Aliwataka
wananchi kukataa kugeuzwa kuku wa kienyeji, ambapo alitoa mfano wa mtu
anayetaka kuwakusanya kuku huwakusanya kwa kuwarushia mtama au pumba,
nao hukimbilia kula bila hata kutaza nyuma au kufikiri.
“Kuna
wenzetu ambao kwa malengo yao maovu wameamua kuwageuza wananchi na
kuwafanya kuku wa kienyeji, wanakuja na fedha zao na wanazitumia
kuwakusanya kwenye viwanja, wananchi kataeni, vinginevyo majuto ni
mjukuu,” alisema.
Tayari
Wasira amekwishapata wadhamini katika mikoa 20, ikiwamo sita ya
Tanzania Visiwani na jana alidhaminiwa katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga
na Geita.
Kwa
mujibu wa utaratibu wa CCM, kila mtangaza nia anapaswa kupata wadhamini
wasiopungua katika mikoa 15 (12 Tanzania Bara na mitatu Tanzania
Visiwani), ambapo jumla ya wadhamini wanapaswa kuwa 450.
Mbali
ya Wasira kutimiza sharti hilo ndani muda wa siku 8, alisema atakwenda
mikoa yote ya Tanzania ili kudhihirishia kuwa amekusudia na ana nia ya
dhati ya kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM, Oktoba, mwaka
huu.
Pia
alitumia fursa hiyo kuwahakikishia Watanzania kuwa yupo imara kabisa
kiakili na kimwili kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika
uchaguzi huo, na kusema kama atateuliwa, basi ataongoza kampeni mwanzo
hadi mwisho bila kutetereka.
Mchakato
wa kuchukua na kurejesha fomu kwa wana-CCM wanaoomba kuteuliwa
utahitimishwa Julai 2, mwaka huu mjini Dodoma, na kufuatiwa na vikao vya
mchujo vitakavyoanza Julai 9.

Comments
Post a Comment