Dar es Salaam.
Mchakato wa kupata wagombea urais kutoka vyama vikuu vya siasa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 umeandika historia ya aina yake baada ya vigogo wanne kujitoa na wengine kuachia nafasi katika vyama vyao ghafla na kuzua mtikisiko.
Vigogo hao ambao ni gumzo kubwa katika majukwaa ya kampeni ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa (2006—2008) na Frederick Sumaye (1995—2005) waliojitoa siku chache baada ya kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha kuwania kuteuliwa na CCM kuwania urais na kujiunga na Chadema, ambako Lowassa alipitishwa kuwa mgombea urais akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kupokewa kwa Lowassa na viongozi wa Ukawa (Chadema, CUF, NCCR – Mageuzi na NLD), kulitarajiwa kuwapa faraja wanachama wao lakini kumesababisha mtikisiko mkubwa baada Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu wadhifa wake akidai nafsi imemsuta na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuachia wadhifa huo na kutangaza kujitoa katika siasa za vyama huku akianzisha mapambano makali dhidi ya chama hicho.
Wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wanasema wanasiasa hao waliofanya uamuzi mgumu wamegundua chama si maisha yao yote, hivyo, wanaweza kuhamia kingine au kustaafu na bado shughuli za siasa zikaendelea.
Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Taasisi ya Hakielimu, Godfrey Bonaventure anasema uamuzi mgumu uliofanywa na Lowassa na Sumaye unaashiria kukua kwa demokrasia.
“Mtu anapoamua kuhama, amegundua kuwa chama si maisha yake yote, anaweza kutafuta sehemu nyingine na kuendeleza safari yake,” alisema.
Alisema uamuzi waliouchukua Lowassa na Sumaye ni mzuri kwani umeongeza nguvu upande wa pili jambo ambalo litakuza demokrasia na kuwasaidia wapinzani kuongeza nguvu na kuufanya uchaguzi wa mwaka huu uwe wa mchuano mkali.
“Kitendo cha Lowassa kuhamia Ukawa ni manufaa kwa upinzani kwani wale wanaohama wanakwenda na wafuasi wao, mbinu za uongozi, wahisani, rasilimali na nguvu mpya. Hata kama hawatashinda, tayari watakuwa wametengeza sura fulani ya ushindani,” alisema.
Alisema uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na mchuano mkali kwa sababu ya Lowassa na Sumaye kinyume na hapo biashara ingekuwa ni ileile.
Kuhusu kujiuzulu nyadhifa kwa Dk Slaa na Profesa Lipumba, Bonaventure anasema kwamba kumepunguza kitu ndani ya vyama vyao na upinzani kwa ujumla ingawa hadhani kama kutaathiri kampeni wala Ukawa.
Credit: Mwananchi
Share with your friends please
Comments
Post a Comment