Blantyre, Malawi. Kipa Ally Mustafa ameibuka shujaa baada ya kuiongoza timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kusonga mbele kwa hatua ya pili ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2018, licha ya kufungwa bao 1-0 na Malawi kwenye Uwanja wa Kamuzu Banda.
Katika mchezo huo wa jana kipa wa Stars, Mustafa ‘Barthez’ alifanya kazi kubwa kupangua mashuti ya washambuliaji wa Malawi katika muda wote wa mchezo.
Dakika ya tisa, kipa Barthez alilazimika kufanya kazi ya ziada kuokoa shuti kali la mshambuliaji wa Malawi, Schumaker Kuwali baada ya walinzi wa Stars kushindwa kumkaba vema nyota huyo.
Malawi ilipata bao la pekee dakika ya 44 lililofungwa na John Banda ambaye alipata mpira akiwa nje ya eneo la 18 na kupiga shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Stars imesonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kuichapa Malawi mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa Jumatano iliyopita na sasa itakabiliana na Algeria katika mechi inayofuata ya kusaka tiketi ya kuingia hatua ya makundi kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2018.
Baada ya mchezo huo kocha wa Stars, Charles Boniface Mkwassa alikiri mechi ilikuwa ngumu na wenyeji walicheza vema kuliko wao, lakini kitu muhimu ni kusonga mbele katika hatua ijayo.
“Tumepigana kadri tulivyoweza na ninawashukuru vijana wangu kwa kujituma sana, lakini kwa mechi hii mambo hayakwenda sawa kama ilivyokuwa katika mechi ya Dar es Salaam. Hata hivyo tunamshukuru Mungu kuwa tumepita kwenda mbele,” alisema Mkwassa.
Licha ya kufuzu, Stars iliponea chupuchupu kutolewa baada ya kutawaliwa kwa muda mwingi wa pambano hilo na wenyeji wao waliokuwa wanacheza kwa kasi wakiwania kupindua matokeo ya Dar es Salaam.
Dakika ya kwanza tu ya mchezo, mshambuliaji nyota wa Stars, Mbwana Samatta alikosa bao la wazi baada ya kuvunja mtego wa kuotea wa walinzi wa Malawi, lakini licha ya kutuliza mpira huo vizuri alipiga shuti hafifu lililodakwa na kipa wa Malawi, Simplex Nthala.
Licha ya kuanza na viungo watatu, Said Ndemla, Mudathir Yahya na Himid Mao, bado Stars ilizidiwa katika eneo la kati huku ikipoteza mipira mingi katika eneo hilo ambalo lilitawaliwa vema na viungo wa Malawi wakiongozwa na Chimango Kayira.
Washambuliaji wa Stars, Samatta na Ulimwengu hawakuweza kuifungua ngome ngumu ya Malawi iliyokuwa ikiongozwa na nahodha Limbikani Mzava ambaye anakipiga katika klabu ya Mpumalanga Aces ya Afrika Kusini.
Malawi walikosa nafasi kadhaa za wazi katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Chiukepo Msowoya na Kuwali mpaka walipopata bao la ushindi lililofungwa na Banda kwa shuti kali la mita 25, ambaye licha ya kucheza winga lakini alileta madhara mara nyingi akiwa katikati.
Kipindi cha pili, licha ya kocha Charles Boniface Mkwassa kujaribu kuongeza kasi ya ushambuliaji kwa kumtoa kiungo Said Ndemla na kumuingiza mshambuliaji John Bocco, huku Mrisho Ngassa akichukua nafasi ya Farid Mussa, bado Stars iliendelea kuwa butu huku kipa Nthala akiwa likizo.
Malawi ilizidisha mashambulizi hasa katika dakika za mwisho, lakini haikufanikiwa kupata bao la pili huku wachezaji wa Stars wakiongozwa na Ulimwengu wakipoteza muda na kumlizimisha mwamuzi Helder De Carvalho Martins kutoka Angola kuwazawadia kadi za njano, Samatta na Ulimwengu kwa kupoteza muda.
Stars inatarajiwa kurejea leo mchana ikitokea jijini Lilongwe baada ya kusafiri alfajiri ya leo kwa mwendo wa kilomita 311 kutoka Blantyre kwenda Lilongwe kwa ajili ya kupanda ndege ya kuwarejesha nyumbani.
Kikosi
Taifa Stars: Ally Mustapha, Shomari Kapombe, Haji Mwinyi, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Himid Mao, Said Ndemla/ John Bocco, Mudathir Yahaya, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samata na Farid Mussa/ Mrisho Ngassa.
Comments
Post a Comment