TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tokea
yalipofanyika Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964, tumekuwa
tukiadhimisha tukio hilo kubwa katika historia ya Zanzibar kila mwaka
inapofika siku hiyo.
Tukio
hilo kubwa ndilo lililopelekea kutangazwa kwa Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume.
Chama
Cha Wananchi (CUF) kimekuwa kikishiriki kikamilifu katika maadhimisho
ya siku hiyo kila mwaka kwa kutambua kwamba Mapinduzi ya tarehe 12
Januari, 1964 ni Mapinduzi ya Wazanzibari wote.
Malengo
makuu ya Mapinduzi hayo yameelezwa na kufafanuliwa vyema kupitia Dikrii
Nam. 6 ya mwaka 1964 iliyopitishwa na Baraza la Mapinduzi ambayo
yanatajwa kwamba ni kuleta usawa, umoja na maridhiano baina ya
Wazanzibari wote na kupiga vita aina zote za ubaguzi.
Tayari
tumetangaziwa kwamba kuanzia tarehe 2 Januari, 2016 kutakuwa na
shughuli mbali mbali zenye lengo la kuadhimisha Mapinduzi yetu na
hatimaye, kama ilivyo ada na desturi, kufikia kilele tarehe 12 Januari,
2016 katika sherehe ambazo zitafanyika Uwanja wa Amaan, mjini Zanzibar.
CUF kama chama cha siasa kinawatakia kheri Wazanzibari wote katika kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi yao.
Hata
hivyo, tunatambua kwamba sherehe za mara hii zinafanyika wakati ambapo
nchi yetu na watu wake wema wamo katika mtihani mkubwa kufuatia kitendo
cha mtu mmoja, Jecha Salim Jecha, kuamua kwa utashi wake na waliomtuma
kuiingiza nchi yetu katika msukosuko na taharuki kwa kudai kwamba eti
ameufuta uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na matokeo yake.
Kwa
kitendo hicho cha mtu mmoja ambaye amevunja Katiba, amevunja Sheria ya
Uchaguzi na amevunja hata maadili ya kazi yake, mara hii nchi yetu
itaadhimisha Mapinduzi huku Serikali ikiwa inaongozwa na viongozi ambao
hawana uhalali na ridhaa ya wananchi.
CUF
tumesisitiza mara zote kwamba hatukubaliani na uamuzi huo wa mtu mmoja
kujinyakulia mamlaka ya wananchi wa Zanzibar yaliyowekwa kikatiba.
Kwa msingi huo huo, tunapenda kutumia fursa hii kuwaeleza wananchi wa Zanzibar kwamba viongozi wetu hawatoshiriki katika shughuli walizopangiwa katika ratiba ya sherehe hizi kwa sababu zifuatazo:
1. Kwa
mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 (Toleo la 2010), Ibara ya
28, Ibara ya 42(2), Ibara ya 48(b), Ibara ya 90(1) na Ibara ya 92(1)
Serikali iliyokuwepo madarakani na Baraza la Wawakilishi lililokuwepo
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2010 – 2015) vilimaliza muda
wake wa uongozi tarehe 2 Novemba, 2015 kwa upande wa Serikali na tarehe
12 Novemba, 2015 kwa upande wa Baraza la Wawakilishi. Kwa sasa, hatuna
viongozi wenye uhalali wa kikatiba kuweza kutekeleza majukumu ya
kiserikali. Kwa hivyo, kushiriki katika ratiba hizo kwa kutumia nafasi
ambazo hazina uhalali tena wa kikatiba ni kwenda kinyume na dhamira ya
waasisi wa Mapinduzi, jambo ambalo hatuko tayari kulifanya.
2. Kiuataratibu,
kilele cha sherehe huongozwa na Rais ambaye yupo kikatiba. Kwa mara ya
kwanza tokea tarehe 12 Januari 1964, sherehe za miaka 52 zitaongozwa na
Rais ambaye ameshamaliza muda wake wa uongozi kikatiba na ambaye hana
uhalali na ridhaa ya wananchi wa Zanzibar. Kushiriki katika sherehe hizo
ni kuhalalisha kipindi cha uongozi ambacho hakipo tena kikatiba. Maalim
Seif Sharif Hamad na viongozi wenziwe ndani ya Chama waliokuweko
Serikalini hadi tarehe 2 Novemba, 2015 hawako tayari kuhalalisha
uvunjaji wa Katiba ya Zanzibar ambayo ndiyo sheria kuu ya nchi.
3.
Viongozi wa CUF wakiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad wanaamini
katika msingi mkuu wa Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 chini ya
uongozi wa Baba wa Taifa la Zanzibar, Marehemu Sheikh Abeid Amani
Karume, ambao ni kuleta utawala wenye ridhaa ya wananchi walio wengi.
Msingi
huo umewekwa wazi na kutiliwa nguvu na Katiba ya Zanzibar ya 1984
(Toleo la 2010) kupitia Ibara ya 9(2)(a) ambapo inaelezwa kwamba,
“Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo
wote wa Serikali kufuatana na Katiba utatoka kwa wananchi wenyewe.”
Mamlaka
hayo ya wananchi yalitekelezwa tarehe 25 Oktoba, 2015 kwa kuwachagua
viongozi watakaoongoza Serikali yao kwa miaka mitano ijayo.
Kitendo
chochote cha kupindua mamlaka hayo ya wananchi ni kwenda kinyume na
misingi ya Mapinduzi na misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa la Zanzibar,
Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume. CUF hatuko tayari kushiriki katika
kuisaliti misingi hiyo na kuisaliti dhamira ya Mzee Karume.
4.
Sherehe za kuadhimisha Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 zina lengo
la kukumbuka malengo ya Mapinduzi hayo na dhamira ya waasisi wake
wakiongozwa na Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume katika kusimamia
utawala wenye ridhaa ya wananchi walio wengi.
Kuzitumia
sherehe za Mapinduzi kuhalalisha utawala usio na ridhaa ya wananchi wa
Zanzibar na ambao haupo kikatiba ni usaliti mkubwa wa dhamira ya kuwepo
kumbukumbu hiyo. CUF hatuko tayari kuwa sehemu ya usaliti huo.
Kwa
sababu hizo zilizoelezwa hapo juu, viongozi wa CUF hawatoshiriki katika
ratiba walizopangiwa mpaka pale chaguo la wananchi wa Zanzibar
walilolifanya tarehe 25 Oktoba, 2015 litakapoheshimiwa.
Tuweke
wazi kwamba tulichoamua ni viongozi wetu kutoshiriki katika ratiba
zinazohusisha viongozi wa Serikali ambao wamemaliza muda wao wa uongozi.
Kwa hivyo, bado tunachukua nafasi hii kuwatakia wananchi wa Zanzibar
maadhimisho mema ya miaka 52 ya Mapinduzi na kuwataka waendeleze umoja,
mshikamano na amani katika nchi.
Mwisho
kabisa, tunamuomba Mwenyezi Mungu awalaze mahala pema Peponi muasisi wa
Mapinduzi yetu, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, na waasisi wenzake
wote na awasamehe makosa yao.
Tunawaomba
Wazanzibari wote kila mmoja kwa dini yake wamuombe Mwenyezi Mungu
kuijaalia kheri na salama nchi yetu na kuyasimamisha yaliyo ya haki.
Tukiishika kamba ya Mwenyezi Mungu hatutoanguka.
Tunawatakia
wote kheri ya mwaka mpya wa 2016 na tunaamini unakuja na kheri kubwa
kwa Zanzibar na watu wake. Ni mwaka ambao safari ya ujenzi wa Zanzibar
Mpya itaanza.
MAPINDUZI DAIMA!
HAKI SAWA KWA WOTE
MANSOOR YUSSUF HIMID
MSHAURI WA KATIBU MKUU – CUF
31 DESEMBA, 2015
Mhubiri afungwa jela maisha Rwanda | Antagon Blog https://t.co/r3fRYx4xCj via @Antagon1
— Antagon1 (@Antagon1) December 31, 2015
Comments
Post a Comment