By Julius Mathias, Mwananchi
Dar es Salaam. Uteuzi wa makatibu wakuu na manaibu wao uliotangazwa juzi na Rais John Magufuli, umepokewa kwa hisia tofauti na wadau wa uongozi na utawala nchini.
Dk Magufuli alitangaza orodha ya watendaji hao waandamizi wa wizara wapatao 50, juzi jioni ambao atawaapisha leo Ikulu.
Dar es Salaam. Uteuzi wa makatibu wakuu na manaibu wao uliotangazwa juzi na Rais John Magufuli, umepokewa kwa hisia tofauti na wadau wa uongozi na utawala nchini.
Dk Magufuli alitangaza orodha ya watendaji hao waandamizi wa wizara wapatao 50, juzi jioni ambao atawaapisha leo Ikulu.
Wachambuzi waliozungumzia uteuzi huo, baadhi wamepongeza mjumuisho wa watendaji hao huku wengine wakiponda wingi wao. Wapo pia walioangazia uwajibikaji wa wateule hao wa mamlaka ya juu nchini.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Omari Mbura alisema Rais ametumia muda mrefu kutafakari watu muhimu na wanaomfaa kumsaidia kuwatumikia Watanzania.
“Kitaaluma na uzoefu haitii shaka yoyote. Hata majukumu yao yamepangwa kutokana na hilo. Watasaidia kuongeza uwajibikaji wizarani,” alisema Dk Mbura na kupongeza jinsi Rais alivyowapandisha vyeo baadhi ya manaibu akisema hilo linasaidia kuongeza morali.
Katika orodha hiyo, Rais amewateua wasomi wa ngazi za uprofesa, udaktari wa falsafa, uhandisi pamoja na watendaji wenye uzoefu wa muda mrefu kwenye utumishi wa umma kama jeshini na taasisi za elimu na afya.
Uteuzi huo umewahusisha majenerali wawili ambao wamekabidhiwa wizara za Mambo ya Ndani na ile ya Maliasili na Utalii.
Licha ya hao, yumo aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Manyara ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi ambaye ameteuliwa kuwa Kaimu Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii ni Meja Jenerali Gaudence Milanzi na Meja Jenerali Projest Rwegasira ambaye pia ni jaji, akipelekwa Mambo ya Ndani. Wakati askari hawa wakipongezwa na kutazamiwa kuongeza mapambano dhidi ya majangili na uhalifu nchini, Maswi ametiliwa shaka.
Aliyekuwa Mbunge wa Kasulu Kusini, David Kafulila alisema mara nyingi uteuzi wa nafasi hizo hutegemea zaidi taaluma na uzoefu alionao mhusika lakini anayeteua ni lazima azingatie uwajibikaji na uadilifu.
“Uteuzi wa Maswi ambaye suala lake bado halijaisha unaleta shaka kidogo... Tutarajie yaleyale,” alisema Kafulila na kuongeza: “Pamoja na upungufu uliopo, lakini utendaji wa wasaidizi hawa wa Rais watatakiwa kuwa kama vile atakavyokuwa aliyewateua. Nchi kama hii ambayo imetoa madaraka makubwa kwa Rais wasaidizi wake hufanya kulingana na afanyavyo yeye (Rais).”
Licha ya kutilia shaka dhana ya kupunguza matumizi ya Serikali, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema anatarajia majenerali walioteuliwa watamaliza changamoto zilizopo kwenye wizara walizokabidhiwa kuzisimamia.
“Ujangili utakwisha na uhalifu pia. Naamini Rais amefanya utafiti na anatarajia msaada mkubwa kutoka kwa watu hawa. Lakini, kwangu mimi, haileti picha kumteua Maswi na kumpa taasisi nyeti ambayo tayari majipu mengi yameshatumbuliwa huko. Hata kama hakuhusika (na sakata la Tegeta Escrow) lakini kuwajibishwa kwake na Bunge kulitosha kumpangia majukumu mengine,” alisema Profesa Mpangala.
Si jambo geni kwa askari kuteuliwa ukatibu mkuu. Aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Omary Mahita alisema hilo limeshatokea mara nyingi na kupongeza kuwa ni suala jema kwani watu hao wanatambua mahitaji ya walio chini yao.
“Alishawahi kuwepo mtendaji wa namna hiyo kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani. Usishangae siku moja Kamishna wa Polisi akateuliwa pia. Mwanajeshi kuwasimamia askari ni ndani ya taaluma yake. Majangili sasa watapambana na askari chini ya uongozi wa askari.”
Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Haki Elimu, Godfrey Bonaventure alimsifu Rais kwa kuzingatia weledi na kuwapangia majukumu wateule wake kwa kigezo hicho na kubashiri kuwa utendaji utaimarika.
Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Haki Elimu, Godfrey Bonaventure alimsifu Rais kwa kuzingatia weledi na kuwapangia majukumu wateule wake kwa kigezo hicho na kubashiri kuwa utendaji utaimarika.
“Uteuzi huu umekuwa safi sana. Acha taaluma itumike kuendesha shughuli za kiserikali. Amejitahidi sana. Hofu yangu ni wingi wao na azma ya kubana matumizi. Naona ni kama yamepunguzwa kwenye nafasi za kisiasa pekee na kuachwa huku,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chama cha CCK, Renatus Muabhi alisema: “Bado elimu siyo kipimo cha uwajibikaji. Wanayo kazi ya kuthibitisha kuwa elimu zao siyo za kwenye vyeti pekee. Hilo litajidhihirisha kwa mafanikio yatakayopatikana ndani ya wizara zao.”
Comments
Post a Comment