Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la
Al-Shabab kutoka Somalia limesema ndilo lililoshambulia ndege
iliyotoboka shimo ikiwa angani mapema mwezi huu.
Kupitia taarifa iliyotumwa kwa barua pepe al-Shabab wamesema shambulio hilo lilikuwa la kulipiza kisasi operesheni za kijasusi zinazoendeshwa na mataifa ya Magharibi nchini Somalia.
Shimo hilo kwenye ndege hiyo lilitoboka muda mfupi baada ya ndege hiyo kupaa kutoka Mogadishu, ikiwa futi 10,000 (3,048m) juu angani.
Ndege hiyo ilifanikiwa kutua kwa dharura.
Ndege hiyo ya shirika la ndege la Daallo, iliyokuwa ikielekea Djibouti, ilikuwa imebeba watu karibu 60.
Maafisa nchini Somalia baadaye walitoa video inayoonesha watu wawili wakimkabidhi abiria mmoja anayeshukiwa kuwa mlipuaji wa kujitolea mhanga kitu kinachoonekana kama Laptop kabla ya mlipuaji kuabiri ndege hiyo.
Msemaji wa serikali anasema kuwa watu hao ndio washukiwa wakuu katika ulipuaji huo.
Inasadikika kuwa mmoja kati ya watu walioleta kipakatilishi hicho alikuwa ni mfanyikazi wa shirika linalohudumu katika uwanja huo wa ndege wa Mogadishu.
Watu 20 wamekamatwa wakiwemo wale wawili walionaswa kwenye video hiyo.
Source: BBC
Comments
Post a Comment