SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), limemthibitisha beki Hassan Kessy kuchezea Yanga katika michuano ya Kombe la CAF CC hatua ya makundi.
Licha ya Kessy pia CAF imetuma leseni ya wachezaji wengine watatu wa Yanga walioongezwa kwa ajili ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) hatua ya makundi, ambao ni Vincent Andrew ‘Dante’, Benno Kakolanya na Juma Mahadhi.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema jana kuwa tayari leseni hizo zimetoka kwa ajili ya wachezaji hao kuitumikia Yanga kuanzia Jumapili ambapo itacheza na Mouloudia Olympique Bejaia ya Algeria. Mchezo huo wa kwanza hatua ya makundi utafanyika Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria.
“Ni kweli tumepokea leseni za wachezaji wanne wa Yanga walioongezwa katika hatua hii, hivyo wote wapo huru kucheza michuano ya kimataifa kuanzia sasa,” alisema Lucas.
Wachezaji hao walijiunga hivi karibuni, ambapo Kakolanya amesajiliwa kutoka Prisons ya Mbeya, wakati Kessy ametoka Simba, Vincent ametoka Mtibwa Sugar na Mahadhi ametoka Coastal Union. Yanga katika kujizatiti na mechi hiyo imeweka kambi yake nchini Uturuki, ambapo imekuwa ikifanya mazoezi chini ya kocha wake Hans Pluijm asubuhi na usiku.
Yanga imepangwa kundi moja na timu za Mo Bejaia ya Algeria, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Madeama ya Ghana.
“Asubuhi hii tulifanya kikao ambapo tuliwaonesha wachezaji wetu baadhi ya mikanda ya video ya mechi za Mo Bejaia. Hivyo wanajua nini watarajie kwa wapinzani wao,” alisema Pluijm, ambaye alikataa kuweka wazi ubora na udhaifu wa wapinzani wao.
Pluijm ambaye yuko na kikosi kamili isipokuwa mshambuliaji Malimi Busungu na beki Juma Abdul, ambao ni majeruhi amekuwa akifanya mazoezi nyakati za usiku kujiandaa na mechi hiyo.
Yanga iliingia kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza kwenye historia ya klabu hiyo baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola kwa mabao 2-1, ikiwa ni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 nyuma kabla ya kufungwa 1-0.
Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi wa Morocco, Bouchaib El Ahrach atakayekuwa katikati akisaidiwa na Redouane Achik na Youssef Mabrouk. Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28.

Comments
Post a Comment