Manchester, England. Kwa waumini wa dini mbalimbali duniani, watashangazwa na kauli ya mshambuliaji wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic.
Mshambuliaji huyo raia wa Sweden aliyetua Manchester United msimu huu akiwa mchezaji huru na kulakiwa kwa kejeli na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Eric Cantona amejibu mapigo kwa kauli inayoshangaza.
Alisema kama Cantona ni Mfalme wa United, yeye ataondoka klabu hiyo ya Old Trafford akiwa ‘mungu’ wa klabu hiyo.
Cantona alimweleza Ibrahimovic kuwa anaweza kuwa mwana mfalme Old Trafford, kamwe hawezi kuyafikia mafanikio yake, yeye ni mfalme.
Lakini, Ibrahimiovic alijibu kwamba mashabiki wa klabu hiyo wasubiri waone na yuko tayari kumziba mdomo Mfaransa huyo mwenye makeke.
Alisema: “Ninamzimia Cantona. Nilisikia yale aliyoyasema. Lakini, siwezi kuwa mfalme wa Manchester. Nitakuwa ‘mungu’ wa Manchester,” limeeleza gazeti la Aftonbladet la Sweden.
Ibrahimovic aliyetoa kauli tata wakati akiondoka Paris Saint-Germain aliongeza: “Nilikwenda kule mfalme, niliondoka nikiwa mkongwe.”
Nyota huyo wa zamani wa Barcelona alitarajiwa kuanza mazoezi na klabu hiyo baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja.
Alieleza dhamira yake ya kuongeza mataji kwenye kabati lake akiwa nayo ya Uholanzi, Hispania, Italia na Ufaransa.
Cantona alimweleza Ibrahimovic alipojiunga na United kuwa ni chaguo sahihi alilolifanya katika maisha yake, lakini kamwe hawezi kuyafikia mafanikio yake.
“Ninao ujumbe maalumu kwake, Zlatan, ameamua kutua hapa, kuvaa jezi nyekundu. Ni chaguo sahihi alilofaya katika maisha yake.
Credit: Mwananchi
