WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Dodoma pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kutenga eneo la bandari kavu ili mkoa huo uweze kupokea na kuhifadhi mizigo na kurahisisha biashara kwa mikoa jirani.
Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Julai 20, 2016) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mkoa wa Dodoma mara baada ya kuweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa awamu ya kwanza ya ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma.
“Ninazo taarifa kuwa Benki ya Dunia kupitia shirika la Local Investment Climate (LIC) tayari wametenga fedha kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kujenga bandari kavu na tayari fedha hizo zimeshapokelewa na Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kazi hiyo.”
“Uzuri wa mkoa wa Dodoma kuna reli. Kwa hiyo makontena yanayoenda Burundi na mahali kwingine yatashushwa hapa na kukaa kwenye bandari kavu; hivyo, wafanyabiashara watachukua mizigo yao hapa badala ya kupata shida ya kuyafuata Dar es Salaam kama ilivyo sasa,” amesema.
Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano itoe wataalam ili washirikiane na CDA kufanikisha kazi hiyo. Amesema hatua hiyo itasaidia kurahisisha wananchi na wafanyabiashara kupata huduma hiyo kwa urahisi na umbali mfupi tofauti na hali ilivyo sasa.
Ameuagiza pia uongozi wa CDA utenge eneo maalum la kituo cha biashara (commercial hub)) ili Kanda zote zinazozunguka mkoa wa Dodoma na nchi jirani wapate bidhaa mbalimbali kutokea Dodoma.
“Kutokana na upanuzi huu na fursa zinazojitokeza, hii iende sambamba na kuwatengea maeneo maalum wajasiriamali badala ya kuwaacha kuzagaa kila mahali,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu upanuzi wa uwanja huo, Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa mradi huo kutaziwezesha ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 90 zianze kutua kwenye kiwanja hicho na kukuza fursa za kibiashara zinazohitaji usafiri wa haraka na salama.
“Katika Ilani ya CCM, suala la ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege limepewa umuhimu mkubwa sana na ndiyo maana leo tunashuhudia utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais ambaye amewezesha upatikanaji wa fedha za ukarabati na fidia kwa wananchi wa kata za Makole na Uwanja wa Ndege ambao maeneo yao yametwaliwa na Serikali ili kufanikisha upanuzi huu,” amesema.
Amesema uzinduzi huo ni mwanzo tu wa utekelezaji wa miradi mingine ya kuboresha na kupanua viwanja vya ndege nchini ambapo Serikali kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato ya ndani na ya nje, itaendelea kuboresha zaidi miundombinu na huduma nyingine za viwanja vya ndege kama vile Mtwara na Mwanza ambavyo amesema vitapanuliwa kufikia hadhi ya kimataifa.
Ameitaja miradi mingine kuwa ni viwanja vya ndege vya Kigoma na Tabora ambavyo vinaendelea kupanuliwa kwa kujenga majengo ya abiria na maegesho ya ndege ili kufikia viwango vya huduma za kimkoa; viwanja vya Shinyanga na Sumbawanga vitapanuliwa kwa kuboreshwa miundombinu na majengo yake kufikia hadhi ya viwanja vya kimkoa; huku kiwanja cha ndege cha Lindi kikiboreshwa miundombinu yake kufikia hadhi ya kimkoa na kuweza kuhudumia viwanda vinavyotokana na uchumi wa mafuta na gesi.
Amesema Serikali itaendelea kukamilisha ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal 3) katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ambalo likishakamilika Desemba 2017 litahudumia abiria wapatao milioni 6 kwa mwaka; ilhali kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) kinapanuliwa miundombinu yake na jengo la abiria ili kiweze kuhudumia abiria milioni 1.2 kwa mwaka.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuhutubia hadhara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa ameiomba Serikali iendelee kuwekeza katika ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato ili ndege za kimataifa ziweze kutua kwenye mkoa huo.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk. Leonard Chamuriho amesema Serikali imetoa sh. bilioni 11.8 kwa ajili ya kazi hiyo na kwamba hadi sasa wamekamilisha asilimia 60 ya ujenzi kwa kuweka lami umbali wa km.2.0 kati ya km.2.5 zinazohitaji kukamilishwa chini ya mradi huo.
Amesema hivi sasa ndege zinazoweza kuruka na kutua kwa umbali huo zinaweza kuanza kutoa huduma kwenye uwanja huo wakati wakiendelea kukamilisha ujenzi wa mita 500 zilizobakia.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Eng. George Sambali alisema ukarabati huo ulianza Juni 24, 2016 na imechukua siku 27 hadi sasa, kazi ambayo alisema inawezesha kiwanja kutumika kwa ndege zenye uwezo wa kubeba abiria hadi 90 na zenye mwendo wa kasi. Hata hivyo, alisema kazi iliyobakia inatarajiwa kukamilika baada ya miezi miwili.